SULUHISHO LA AJIRA KWA VIJANA NA FURSA ZILIZOPO

Katika utafiti uliofanyika hivi karibuni umegundua changamoto ya ajira kwa vijana imeongezeka kwa kiasi kikubwa, Asilimia 70 ya vijana wenye miaka kati ya 13 na 34 ambao ni wengi zaidi kati ya idadi ya watu Milioni 62 waliopo Tanzania kutokana na sensa iliyofanyika mwaka 2022, Hii inafanya Tanzania kuwa na kundi kubwa ambalo ni tegemezi, Hapa ndio linakuja swali, Je, nini kifanyike kutoa suluhisho la ajira kwa vijana? Na Je, Fursa zinatolewa za kutosha ili vijana wajiajiri na kujikwamua kiuchumi?
Vijana zaidi ya 850,000 wanahitimu masomo kila mwaka huku wakiwa tayari kuingia kwenye soko la ajira lakini kati yao wanaopata ajira ya kudumu ni asilimia 5 tu na asilimia 35 ikijikita katika kilimo ambacho bado kinakabiliwa na changamoto nyingi, Hivi sasa vijana zaidi ya elfu 30 wanahitimu katika vyuo mbalimbali na wengi wakiishia mutaani kwa kukosa ajira. Hawa elfu 30 ni wale ambao walifanikiwa kupenya darasa la saba, kidato cha nne na sita, Maana yake ni kwamba wapo vijana wengi walioshindwa kuendelea na masomo kutokana na sababu mbalimbali.
Wapo walioishia darasa la saba na kuingia mitaani, na wapo walioishia kidato cha nne na sita na kuishia huko mitaani, wakiwa hawana ujuzi wowote.
Tatizo la ajira nchini kwa kiasi kikubwa ni matokeo ya mfumo mbovu wa elimu ambao unazaa vijana wengi wasio na uwezo wa kuajiriwa popote na hata kujiajiri. Kwa sasa hali ni mbaya sana kwa sababu hata wanaomaliza vyuo vikuu wanakosa maarifa na asilimia kubwa husubiri kuajiriwa katika nchi ambayo kwa mwaka inatengeneza ajira kwa kiasi kidogo sana.
JE, Nini kifanyike kusuluhisha tatizo la ajira kwa vijana?
Elimu bora inayokidhi mahitaji ya taifa
Hii ndio nyia mojawapo ya kutatua tatizo la ajira nchini kwani fursa za ajira zipo duniani kote ila wanaozifaidi ni wale wenye maarifa na ujuzi ambao msingi wake ni elimu bora wanayoipata. Endapo mfumo wa elimu ukibadilishwa utaongeza wigo mkubwa wa vijana wanaotoka vyuoni kujiajiri badala ya kusubiri kuajiriwa, hii haitokua na msaada kwao tu bali Taifa kwa ujumla na kupunguza utegemezi.
Nchi imelala kwenye sekta ya viwanda.
Kama tujuavyo sekta ya viwanda ndio inayoweza kuajiri watu wa aina yoyote, Wenye ujuzi na wasio na ujuzi, Wenye elimu na wasio na elimu, Kuimarisha sekta ya viwanda maana yake ni kuinua sekta ya kilimo ambayo ni eneo muhimu la kutatua tatizo la ajira, Kwa kujenga uchumi wa viwanda maana yake utahitaji malighafi ambazo zinazalishwa hapa nchini. Kujenga viwanda vya kubangua korosho maana yake unawahamasisha wananchi kulima kwa wingi zao la korosho maana unawahakikishia soko la korosho zao. Pia kujenga viwanda vya kusindika matunda maana yake unawahamasisha wananchi walime kwa wingi matunda.
Kuwasimamia vijana waliojiajiri kwenye biashara ndogondogo.
Vijana waliowekeza fedha zao kwenye biashara ndogo na za kati wasimamiwe ipasavyo kwenye biashara zao, Tumeshuhudia mara kadhaa vijana waliodunduliza “visenti” vyao na kufungua biashara zao pembezoni mwa barabara kwa lengo la kujipatia riziki wanafukuzwa na kubomolewa mabanda yao na kuwapeleka maeneo mbadala, wakati mwingine wakipelekwa maeneo ambayo aidha hayana miundombinu au yapo mbali na makazi ya watu.